FALSAFA MPYA YA MAISHA; KWA NINI TANO(5), Njia Ya Uhakika Ya Kutatua Tatizo Lolote Ulilonalo.

On Sun, Sep 4, 2016 at 11:18, Nsolo S. Stephen
<nsolo_stif@yahoo.com> wrote:

On Sun, Sep 4, 2016 at 9:08, AMKA MTANZANIA
<makirita@kisimachamaarifa.co.tz> wrote:

Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?

Hongera kwa kuendelea kutengeneza falsafa ya maisha yako, ili uweze kuwa na msingi imara wa kufanya maamuzi muhimu ya maisha yako. bila ya kuwa na falsafa, bila ya kuwa na kitu unachosimamia, utakuwa unapelekwa na kila kitu kama bendera inavyopelekwa na upepo. Hayo siyo maisha mazuri, kwani utajikuta unapoteza muda na hupati kile ambacho unakitaka.

Karibu kwenye makala yetu nyingine ya falsafa ya maisha leo, na tutakwenda kuangalia kwa kina namna tunavyoyatatua matatizo letu. Kumekuwa na tatizo juu ya tatizo, yaani mtu anakuwa na tatizo, halafu anakuwa na tatizo la kutatua tatizo alilonalo. Hii imekuwa inasababisha watu kufanya makosa zaidi na hivyo kukuza matatizo waliyokuwa nayo.

Kuna usemi kwamba kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua, usemi huu umebeba ukweli mkubwa mno, lakini ni wachache sana ambao wamekuwa wanauzingatia. Watu wamekuwa wakiparamia matatizo ambayo hawajayajua vizuri na hivyo kukwama kwenye njia wanazotumia kuyatatua. Watu wamekuwa wanasikia kitu juu juu na kukimbilia kuchukua hatua kabla hata hawajajiridhisha na taarifa walizopata, badala yake wamekuwa wanajikuta wakitengeneza matatizo makubwa zaidi ya waliyokuwa nayo awali.

Abraham Lincolin, aliyekuwa raisi wa Marekani amewahi kunukuliwa akisema, ukinipa masaa sita ya kukata mti, nitatumia masaa manne kunoa shoka langu. Ukiangalia kauli hiyo kwa juu, unaweza kusema huyu bwana Lincolin alikuwa mtu mvivu sana, badala aanze kuhangaika kukata mti yeye ananoa shoka muda wote huo? Lakini utakapoangalia kwa undani, ni shoka lipi linakata mti kwa urahisi? Shoka kali au shoka butu?

Watu wengi kwenye maisha wamekuwa wanaparamia miti yao na mashoka ambayo ni butu, wanakazana kukata lakini hawafanikiwi kuangusha miti wanayokata. Kwenye mfano huu, mti unaweza kuwa matatizo yetu na shoka akili zetu.

Hivyo basi kwenye makala yetu ya leo ya falsafa mpya ya maisha, tunakwenda kujifunza namna tunavyoweza kunoa mashoka yetu ili tukate miti yetu vizuri na kwa haraka. Tunakwenda kujifunza namna tunavyoweza kutumia akili zetu vizuri ili kupata njia bora ya kutatua matatizo tunayokutana nayo kwenye maisha yetu.

Kama tulivyoona hapo juu, kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua, hivyo kabla hatujakimbilia kuchukua hatua, lazima kwanza tulijue tatizo. Na sio tu kulijua, badala yake tulijue nje ndani, tulijue kwa uhakika na tusiache hata eneo moja ambalo hatujalijua vizuri.

SOMA; Rasilimali Mbili Muhimu Unazohitaji Ili Kuwa Bora…

Je unawezaje kulijua tatizo lolote kwa undani ili uweze kulitatua?

Hapa ndipo inakuja njia ya kutumia KWA NINI TANO, kwa njia hii unajiuliza kwa nini mara tano kwenye tatizo lolote unalokutana nalo. Unapojiuliza kwa nini mara tano, unajilazimisha kufikiri kwa kina ili kuja na majibu sahihi kwa hali yoyote unayopitia.

Kwa kujiuliza kwa nini tano, utafika kwenye kiini au mzizi wa tatizo unalopitia na hivyo kulitatua kwa njia ambayo ni ya uhakika na kuweza kupata majibu mazuri.

Hebu tuchukue mfano wa kipato kuwa hakitoshelezi.

Kwa njia ya kawaida ya kutatua tatizo la kipato kutokutosheleza, watu huwa wanaangalia kwa sasa hawana fedha za kutumia, wanajiuliza kwa nini na jibu wanalopata ni mshahara hautoshi, hivyo wanakwenda kukopa ili kupata fedha wanazotaka kwa sasa, na wakati huo wanakwenda kwa waajiri wao na kuomba waongezewe mshahara. Kwa njia hii wanakuwa na madeni, na wakati huo pia mshahara hauongezeki. Kinachofuatia ni kulaumu na kulalamika kila siku kwamba kipato hakitoshi.

Sasa tuangalie njia ya kutumia KWA NINI TANO ili kutatua tatizo la kipato kutokutosheleza.

  1. Kwa nini nina tatizo la fedha?

Kwa sababu matumizi yangu ni makubwa kuliko kipato changu.

  1. Kwa nini kipato changu ni kidogo kuliko matumizi?

Kwa sababu mshahara wangu ni mdogo.

  1. Kwa nini mshahara wangu ni mdogo?

Kwa sababu nafanya kazi za ngazi ya chini au kile ninachofanya kila mtu anaweza kufanya hivyo hata nikiondoka wengine watapatikana.

  1. Kwa nini nafanya kazi za ngazi ya chini ambapo nalipwa kidogo?

Kwa sababu sijajiendeleza kwa muda mrefu, nimekuwa nafanya kazi zangu kwa mazoea, hakuna kikubwa na cha tofauti ninachofanya.

  1. Kwa nini sijiendelezi kwenye kazi yangu?

Kwa sababu sijaona umuhimu huo, au nimekuwa mvivu kutenga muda wa kufanya hivyo. Na kwa kushindwa kujiendeleza nitaendelea kubaki hapa hapa.

Hitimisho; ili kutoka hapa kwenye tatizo la fedha, nahitaji kujiendeleza kwenye hii kazi ninayofanya, nahitaji kuifanya kwa utofauti na kuepuka mazoea na pia nahitaji kuangalia mapato na matumizi yangu yasitofautiane, nihakikishe kwa sasa matumizi yangu yanakuwa chini ya mapato yangu.

Kwa mfano huo hapo juu unaona jinsi ambavyo umechimba ndani na kuja na suluhisho ambalo litakutoa hapo ulipo, kuliko njia ya awali ambayo ungepata suluhisho lisiloweza kukusaidia.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Hii Hapa Ni Njia Iliyo Wazi Kabisa Kwako Kufikia Mafanikio Makubwa.

Unaweza kutumia njia hii ya KWA NINI TANO kwenye kila jambo kwenye maisha yako, ni njia bora kabisa ya kutatua matatizo na changamoto zako.

Akili zetu zina uwezo mkubwa sana wa kutatua tatizo lolote tunalopitia, tatizo huwa hatuzishughulishi hivyo zinapumzika. Lakini unapoilazimisha akili yako kuja na majibu kuhusu kile unachopitia, lazima itakuja na majibu ambayo ukiyafanyia kazi hali yako itabadilika.

Changamoto yoyote inayokusumbua kwenye maisha yako, hebu ipitishe kwenye kwa nini hizi tano, utaona njia nyingi za kuitatua changamoto hiyo.

Ongeza zana hii muhimu kwenye falsafa yako mpya ya maisha, kama walivyo wanafalsafa wote, usiache kuhoji na kujihoji. Kila kitu kinapaswa kuhojiwa, tumia kwa nini tano kupata ukweli wa jambo lolote unalotaka kupata ukweli wake.

Nakutakia kila la kheri katika kujijengea falsafa hii mpya ya maisha, kumbuka maisha ni falsafa, bila ya falsafa, maisha yatakuwa hovyo mno.

TUPO PAMOJA,

KOCHA MAKIRITA AMANI.

www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Kwa ushauri na Coaching bonyeza maandishi haya kupata utaratibu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s